Jumatano, 29 Mei 2013

Balozi Seif atembelea Chuo cha Afya, Wawi

 Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Dr. Salhia Muhsin Ali akitoa maelezo mbele ya Kikao cha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Wanafunzi wanaosoma mafunzo ya Udaktari katika Chuo cha Afya waliopo Wawi Kisiwani Pemba
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wanafunzi  12 wa Chuo cha Afya wanaosomea fani ya Udaktari waliopo Kisiwani Pemba.
 Rais wa Wanafunzi wa chuo cha afya waliopo Kisiwani Pemba Ali Omar Khalifa akitoa baadhi ya changamoto zinazowakabili wanafunzi wa chuo cha afya waliopo Kisiwani Pemba.
 Mwalimu Mkuu wa Wanafunzi wa Chuo cha Afya waliopo Pemba Dr. Maria Makdalema akielezea furaha yake kutokana na umahiri wa wanafunzi wake mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipowatembelea kwenye makazi yao Wawi Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mwalimu Mkuu wa Wanafunzi wa chuo cha Afya waliopo Kisiwani Pemba Dr. Maria Makdalema.
Pembeni yao ni Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Mkasha Hija Mkasha na Mkurugenzi  Idara ya Tiba Zanzibar Dr. Salhia Muhsin Ali.(Picha na Hassan Issa, OMPR.)
.................................................

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kumgharamia mwanafunzi yeyote atakayeamua kujiongezea  taaluma ya fani yoyote ya Udaktari Bingwa kwa lengo la kuiondoshea Zanzibar uhaba wa Madaktari.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wakufunzi pamoja na Wanafunzi wa chuo cha afya wanaosomea fani ya Udaktari chini ya Wataalamu wa Cuba hapo Wawi chake chake Pemba.
Balozi Seif alisema uwamuzi huo wa serikali umelenga kukidhi ule Mpango wake uliojipangia wa kuimarisha huduma za Afya katika kila umbali wa Kilomita Tano katika Visiwa vya Zanzibar.
Alisema Serikali katika kukabiliana na upungufu wa Madaktari bingwa wa fani tofauti imetowa fursa hiyo ili Daktari mwenyewe awe huru kuamua kuongeza ujuzi zaidi katika Nchi na fani aiwezayo huku akilenga kuja kuisaidia Jamii yake mara amalizapo mafunzo hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wanafunzi hao kwa ushiriki wao wa mafunzo hayo ya miaka saba na kuelezea matumaini yake kwamba wamalizapo mafunzo hayo ni kutoa huduma kwa kuzingatia maadili ya Udaktari.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kuwa na Madaktari 50 kwa mpigo jambo ambalo ni mafanikio makubwa  kwa Serikali “. Alionyesha furaha yake Balozi Seif.
“ Historia ya kuanzishwa kwa darasa la Madaktari Zanzibar limetokana na ziara ya Dr. Sheni  Nchini Cuba wakati akiwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya  Muungano wa Tanzania katika miaka ya 2008 “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba wazo hili lililotolewa na Cuba lilikuwa na nia ya kusaidia gharama za usomeshaji ambazo ni kubwa pamoja na udhibiti wa wanafunzi hao ambao wakisoma nje ya nchi wanakuwa na mawazo ya kuikimbia nchini.
Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar ameahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaangalia na kuimarisha mazingira ya walimu pamoja na wanafunzi hao ili waweze kufanikisha lengo lililokusudiwa chuoni hapo.
Alisema haipendezi kuona wataalamu hao wamekubali kujitolea kusaidia wananchi wa Tanzania na Zanzi bar kwa ujumla na mazingira yao hasa makazi yanakuwa hayako katika hali ya kuridhisha.
Wakitoa baadhi ya changamoto zinazowakabili Wanafunzi hao wa Udaktari walisema upungufu wa vifaa limekuwa tatizo sugu linalorejesha nyuma mafunzo yao ya kila siku.
Waliiomba Serikali kupitia Wizara ya afya kuyafanyia kazi matatizo hayo likiwemo pia tatizo la  mtandao wa Internet kwa wakufunzi wao sambamba na usafiri wanakwenda na kurudi kwenye mazoezi hasa wakati wa usiku.
Wanafunzi hao wa Udaktari wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake huo wa kuanzisha mafunzo hayo hapa Nchini ambao utapunguza gharama kubwa.
Naye kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Darasa hilo Dr. Maria Makdalema kutoka Nchini Cuba ameelezea furaha yake kutokana na umahiri mkubwa walionao wanafunzi wake.
Hata hivyo Dr. Maria alisema `ukosefu wa vifaa vya mazoezi unawapa mazingira magumu wanafunzi hao katika kujipatia mazoezi ya vitendo ambayo ni muhimu katika mafunzo yao.
Mapema Mkurugenzi Idara ya Tiba ambae ndie anayeratibu mafunzo hayo Dr. Salhia Muhsin Ali alisema mafunzo hayo ya Udaktari yamejumuisha wanafunzi 50 ambao 38 kati yao wapo Unguja na 12 Kisiwani Pemba.
Dr. Salhia alieleza kwamba wanafuzi 38 wa Unguja hivi sasa wako katika hatua ya mwisho kumaliza mafunzo yao ya miaka saba wakati wale 12 wa Pemba wanaingia mwaka wa nne wakiwa katika mkupuo wa tatu.
Katika Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alichangia shilingi Laki Tano kusaidia ununuzi wa Vifaa muhimu vidogo vidogo na kuahidi Serikali Kuu kuyafanyia kazi yale matatizo mengine makubwa likiwemo lile la upatikanaji wa Projector.
VIA/www.zanzinews.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...