Wizara ya
Maliasili na Utalii imeanza mikutano ya mchakato wa kupokea maoni
kutoka kwa watu na makundi mbalimbali kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka ya
Wanyamapori (TAWA).
Mkutano
wa kwanza umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Chuo cha
Taifa cha Utalii kampasi ya Bustani kwa kuanza kupokea maoni kutoka kwa
viongozi waliowahi kuwa mawaziri,makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara
kuhusu uanzishwaji wa Mamlaka hiyo.Akizungumza
kuhusu hatua hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis
Kagasheki wakati akifungua mkutano huo alisema Sheria ya Wanyamapori ya
Mwaka 2009 inaitaka Wizara kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori kazi ambayo
itakamilika Novemba mwaka huu.
Mhe.
Waziri alisema kuwa Wizara kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji
imeamua kuanza na viongozi waliowahi kuitumikia Wizara ili waweze kutoa
maoni juu ya Sheria na Muundo wa Mamlaka ya Wanyamapori pamoja na Sheria
ya Idara ya wanyamapori itakayobaki katika Wizara.
"Nyalaka
hizi zimetengenezwa na watu wa ndani ya Wizara wenye uzoefu wa muda
mrefu na hivyo tumeona ni vizuri tuwashirikishe ninyi viongozi mliowahi
kuitumikia Wizara ili muweze kutoa michango yenu itakayotuwezesha kupata
kitu bora kitakachopelekwa katika Baraza la Mawaziri na kisha kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ili Bunge la Novemba tuweze kuiwakilisha
ikiwa ina baraka na maoni kutoka kwa kamati ya Bunge ili ipitishwe kama
Sheria ya Mamlaka ya Wanyamapori," alisema Mhe. Waziri.
Kuanzishwa
kwa Mamlaka ya Wanyamapori kutasaidia katika kurahisisha usimamizi wa
rasilimali watu, kujitegemea kimaamuzi, na kuwa na uwezo wakujiendesha
yenyewe bila kutegemea fedha kutoka hadhina.
Miongoni
mwa mawaziri waliohudhuria mchakato huo ni Mhe. George Kahama, Mhe.
Getruda Mongella, Mhe. Ezekiel Maige, Mhe. Dkt. Juma Ngasongwa, Mhe.
Zabehi Mhita na Mhe. Arcado Ntegazwa.
Makatibu
wakuu waliofika ni Mhe. Philimon Luhanjo, Mhe. Marten Rumbanga, Mhe.
Rose Lugembe, Mhe. Balozi Dkt. Ladislaus Komba, Mhe. Alhaj Muhidin
Ndolanga, Mhe. Salehe Pamba na waliowahi kuwa wakurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori.
PICHANI
MBELE NI WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AKIWA NA WALIOWAHI KUWA MAWAZIRI
WA WIZARA HIYO NA MSITARI WA NYUMA NI WALIOWAHI KUWA MAKATIBU WAKUU
WAKIFUATIWA NA WALIOWAHI KUWA WAKURUGENZI WA IDARA YA WANYAMAPORI NA
MAOFISA WAANDAMIZI WA SASA WA IDARA YA WANYAMAPORI.
TulizoKilaga,
Information Officer,
Ministry of Natural Resources and Tourism,
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni