Na Francis Godwin, Njombe
WAKATI kukiwa na vugu vugu ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) kwa baadhi ya madiwani na wabunge kuacha kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi waliowachangua na badala yake kufanya kazi ya kujihami na wale wanaonyemelea majimbo na kata zao ,katibu mkuu wa CCM Taifa Abdalrahman Kinana ametoa onyo kali kwa madiwani na wabunge hao wasio watumikia wananchi kuwa wasije kulalamika mbele ya safari.
Huku akiwapasha wana makada wa CCM wanaojipitisha katika majimbo ,kata na nafasi za urais kuwa wanapoteza muda wao bure kwani muda wa kampeni bado na kuwa kufanya kampeni kabla ya muda ndani ya CCM ni kosa na pale itakapobainika wataenguliwa katika nafasi ya ugombea kutokana na kukosa sifa na kukiuka taratibu za chama.
Kinana alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wana CCM na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Rudunga wilaya ya Wanging'ombe mkoni Njombe .
Alisema kuwa kazi kubwa waliyopewa madiwani na wabunge ni kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM pamoja na kuwawakilisha vema wananchi na iwapo viongozi hao watajikita zaidi katika kuendelea kutetea nafasi zao bila kuwatumikia wananchi waliowachagua basi watakuwa hawatoshi kuendelea kushika nafasi hiyo.
" Madiwani na wabunge huu ni wakati wao wa kuwatumikia wananchi waliowachagua si wakati wa kuendelea kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo muda bado haujafika wa kuanza kampeni....pia nawaombeni kampeni zenu ziwe za kuwatumikia vema wananchi ili muda ukifika wananchi waweze kukuchagua kwa kazi nzuri uliyoifanya na si kwa kazi ya kutafuta utukufu badala ya utumishi"
Aidha Kinana alisema kuwa CCM hakitafanya kosa ya kuwapoteza wabunge wake wazuri ambao wamekuwa wakifanya kazi zinazoonekana kwa wananchi katika majimbo pamoja na madiwani wanaokubalika kwa wananchi kwa kazi zao.
Huku akisisitiza suala la wale wote waliochaguliwa na wananchi na kupewa nafasi ya kusimamia ilani ya CCM kuepuka kufanya kazi kwa misingi ya kutafuta heshima badala ya kuwatumikia wananchi waliomchagua.
"Nawahakikishia wana CCM na wananchi kuwa hatutafanya kosa katika kuwateulia wana CCM wanaokubalika na wale ambao hawakubaliki kwenu na kwetu pia hatutawakubali kamwe"
Hata hivyo Kinana aliwataka viongozi wa CCM wakiwemo wabunge na madiwani kurudisha mrejesho kwa wananchi wao juu ya kazi waliyoifanya na kusimamia na kutekeleza ilani ya CCM na pale ambapo wameshindwa kutekeleza wasiogope kuwaeleza ukweli sababu za kushindwa na kudai kuwa CCM si chama cha miujiza ambacho kinauwezo wa kutekeleza kila jambo kwa wakati.
Wakati huo huo Kinana amewachangia kiasi cha shilingi milioni 10 vijana wa kijiji cha Mlangali kata ya Ruduga wilaya ya Wanging'ombe kwa ajili ya kuwawezesha kuanzisha chama cha ushirika cha kuweka na kukopa (SACCOS) ili kuwasaidia kukopeshana fedha za miradi ya kimaendeleo.
Kinana alisema lengo la kuwasaidia fedha hizo ni kutokana na kufurahishwa na jitihada mbali mbali za uzalishaji maji zinazofanywa na vijana wa kijiji hicho kupitia mradi wa umwagiliaji uliopo katika eneo hilo na hivyo fedha hizo zitawawezesha kupiga hatua zaidi na kuwasaidia wenzao wasio na mitaji kujiunga katika kikundi hicho na kukopeshwa kwa taratibu watakazoona zinafaa.
Pia aliwaahidi mizinga ya nyuki 25 wanachama wa jumuiya ya wazazi kijiji cha Mlangali ili kuendeleza shughuli ya ufugaji wa nyuki na kuchangia mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya umaliziaji wa ofisi ya CCM kijiji cha Mlangali
Katika ziara hiyo wilaya ya Wanging'ombe jumla ya wanachama zaidi ya 100 kutoka vyama vya upinzani kikiwemo Chadema, CUF, TLP na wengine wasiokuwa na chama walijiunga na CCM wakiwemo waliokuwa viongozi wa Chadema wilaya hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni