Jumatano, 12 Juni 2013

VITA DHIDI YA UJANGILI: BALOZI KAGASHEKI APULIZA KIPYENGA

DSCF1536 4476b
Waziri wa maliasili na utalii, Balozi Hamis Kagasheki akifungua mkutano wa TANAPA na wahariri wa habari wa vyombo mbalimbali nchini unaofanyika kwenye ukumbi wa Siasa ni kilimo, Manispaa ya Iringa.  
DSCF1546 d93ef
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, maliasili na utalii akizungumza kwenye mkutano huo
DSCF1529 9c9da
Mkurugenzi wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi akizungumza kwenye mkutano huo
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamisi Kagasheki, amepuliza kipenga. Kilichobaki sasa ni kwa wachezaji kushiriki kikamilifu kupambana na ujangili, kwani mambo yameoza na yanahitaji kusafishwa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya wahariri wa habari nchini iliyofanyika leo mjini Iringa, Balozi Kagasheki amesema wimbi la ujangili linazidi kuongezeka kila kukicha kiasi cha kutishia uwepo wa Tembo pamoja na viumbe wengine, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu mapambano hayo.
“Things are rotten and should be cleaned up (mambo yameoza na yanahitaji kusafishwa),” amesema Waziri Kagasheki. “Nini waandishi ni wachezaji katika vita hii, ingawa mwisho wa siku Serikali ndiyo yenye wajibu mkubwa wa kupambana na janga hili. Mchango wa wanahabari ni muhimu sana.”
Balozi Kagasheki amesema, vita dhidi ya ujangili haiwezi kuonewa haya na akatoa rai kwa wanahabari kutumia taalamu yao kufichua maovu yote yanayohusiana na ujangili na kuutokomeza, vinginevyo vizazi vijavyo vitawahukumu.
Amesema vyombo vya habari visisite kuwafichua wahusika, hata kama waziri mwenyewe yumo kwenye mtandao huo, kwani maslahi ya taifa ni ya kupewa kipaumbele.
Akizungumzia ukubwa wa tatizo hilo, Balozi Kagasheki amesema haiyumkini kwa pembe za ndovu kukamatwa ng’ambo wakati makontena hayo yanajazwa na kusafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam, hali ambayo inaleta taswira kwamba hata watumishi wa umma wanahusika kwa kiasi kikubwa.
“Pale bandarini kuna polisi, kuna customs (forodha), kuna TPA wenyewe, na kuna maofisa wa usalama. Inakuwaje basi meno haya ya tembo yanapakiwa pale na kusafirishwa, halafu yanakwenda kukamatwa Hong Kong, au Philippines, au Vietnam. Hapa kuna tatizo, lazima tuliseme,” amesema.
Amesema rushwa kwa watumishi wa umma na waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali hizo ni kubwa, hali inayoifanya vita hiyo kuwa ngumu.
Hata hivyo, amesema kuongezeka kwa ujangili kunachangiwa na mambo mengi, yakiwemo mahitaji ya meno ya tembo ulimwenguni, faida itokanayo na biashara hiyo kuwa kubwa, umaskini wa wananchi, na mmomonyoko wa maadili kwa watumishi wa umma.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, amesema pamoja na vita hiyo kuwa ya muda mrefu, lakini inakuwa vigumu kwa vile wahusika ni watu wenye fedha na hawaogopi kupoteza chochote.
Amesema wanahabari wanatakiwa kutokuwa waoga hata kama wanaopambana nao ni watu wenye fedha.
“Msiogope hata kama hawa wana mapesa, vita hii ni kubwa na tunapaswa kupiganwa kwa nguvu zote kuhakikisha tunatetea maliasili ya taifa,” amesema.
Hata hivyo, amepinga takwimu za TAWIRI kuhusu idadi ya tembo wanaouawa kila siku na kusema mara nyingi takwimu hizo zinatengenezwa na maofisa kuilinda serikali huku katika uhalisi tatizo hilo likionekana kuwa kubwa zaidi.
“Hizi takwimu siyo sahihi na zaidi zimejikita kwenye maeneo yale tu yaliyo chini ya hifadhi, vipi kuhusu maeneo mengine ambayo hayatambuliki? Kwa hiyo, idadi ya tembo wanaouawa kila siku inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko tunavyoelezwa,” amesema.
Lembeli amesema Idara ya Maliasili haina watumishi wa kutosha, bajeti ni ndogo na maslahi ni duni, hivyo kuitaka serikali, kama kweli imedhamiria kukabiliana na tatizo hilo, basi iongeze watumishi na kuwamotisha.
Amewataka wahariri hao wa habari kuunda Jukwaa la Marafiki wa Big Five (Friends of the Big Five) litakalowashirikisha wadau mbalimbali kuanzisha mijadala ya namna ya kupambana na ujangili pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, ameitaka serikali kuongeza kasma kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kama ilivyofanya katika sekta ya madini miaka kadhaa iliyopita.
“Sekta ya madini ilitengewa fedha nyingi zaidi, lakini hivi sasa wametuachia mashimo. Sasa ni wakati wa serikali kuitengea fedha nyingi idara ya utalii na maliasili kwa sababu kuna uhakika wa kuongezeka maradufu kwa pato la taifa kutoka asilimia 17 ya sasa,” alisema. Chanzo: mjengwablog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...