Jumanne, 9 Julai 2013

RAIS ATOA RISALA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akitoa risala ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa wananchi ,huko Ikulu Mjini Zanibar leo mchana.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar haitovumilia kuona watu wanahatarisha maisha na afya za wengine kwa kuwauzia bidhaa zilizopitwa na wakati, mbovu,bei ya juu na zisizokuwa na vipimo bora hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema
hayo leo katika risala ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani aliyoitoa kwa wananchi
kupitia vyombo vya habari
Katika risala hiyo kwa wananchi, Dk. Shein alisema kuwa wakati watu wanatafuta riziki katika mwezi huu wanapaswa kuzingatia haki na kurehemiana sana katika biashara, hasa
muuzaji na mnunuzi.
Alisema kuwa inafahamika kuwa faida kwa mfanyabiashara ni lazima, ili aweze kujimudu na
kuendelea lakini wakati huohuo akumbuke kufanya biashara bila ya kupitisha
hadaa.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein aliviagiza vyombo husika kuchukua hatua madhubuti
kuhusu masuala hayo ya biashara sambamba na mazao ya kilimo, kama vile ndizi
zinazouzwa sokoni zikiwa changa.
“Inafaa tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia Baraka ya mazao ya aina nyingi ya
kilimo wakati huu na vile vile nawashukuru wafanyabiashara wetu kwa kujaza
madukani mwao bidhaa mbali mbali zinazohitajika zaidi katika mwezi huu,
zikiwemo vyakula na nguo”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kurehemeana kwa njia mbali mbali hasa
katika kutoa sadaka kwa kuwasaidia wale wasiojiweza, mayatima, masikini, wanafunzi
waliopo daghalia, wagonjwa waliopo hospitali pamoja na watu wengine wanaotaka
kusaidiwa angalau kwa futari.
Dk. Shein aliwataka wananchi kuzifuata taratibu zote anazotufunza Mwenyezi Mungu na
Mtume wake ikiwa ni pamoja na kuondoa sababu zote za utengano na mfarakano na
badala yake waimarishe umoja, mshikamano, ihsani na kupendana.
Dk. Shein alisisitiza kuwa Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani umekuja wakati wa msimu
wa utalii nchini hivyo ni vyema kuwa na subira na kuwaongoza wageni juu ya
taratibu, mila na kanuni zilizopo nchini katika mwezi huu wa Ramadhani bila ya
bughudha au uvunjaji wa sheria.
Aliwafahamisha wafanyabiashara wa vyakula, mahotelini na mikahawani kuwa wanapaswa kuheshimu khulka, mila na utamaduni wa Zanzibar na kutofanya mambo ya karaha yatakayopelekea kuwakasirisha wanaofunga. 
Dk. Shein aliwataka wasiofunga kuwaheshimu wanaofunga na hatimae kuifanya Ramadhani
iwe ni kivutio cha wageni kwa utamaduni na ustaarabu wa Zanzibar. 
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Mamlaka ya Maji Zanzibar
(ZAWA) itafanya kila juhudi ili kuhakikisha kuwa maji yanapatikana katika
maeneo mbali mbali hapa nchini.
Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kuwa waangalifu na kutumia vyakula na maji
bila ya israfu.
Katika risala hiyo Dk. Shein alimuomba MwenyeziMungu kuijaalia Ramadhani kuwa yenye
mafanikio, kuanzia kwa wafanyabiashara, wakulima, wavuvi, washoni, waendeshaji
darsa za dini, vijana, wazee na wananchi wote kwa jumla. 
 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822   
  E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...