CHAMA cha Mapinduzi CCM
wilaya ya Gairo kimeitaka wizara ya maji kuwapa majibu sahihi na ya uhakika juu
ya lini mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia utakamilika
na wananchi wa wilaya hiyo kuondoakana na kero kubwa ya maji inayowakabili.
Mwenyekiti wa CCM wilaya
Hiyo Omar Awadhi alisema hayo jana wakati wa ziara ya katibu wa CCM mkoa wa
Morogoro Rojas Romuli na viongozi wa CCM wilaya hiyo kutembelea mradi huo
uliopo katika kata ya Gairo.
Awadhi alisema kuwa pamoja
na ahadi aliyoitoa waziri wa Maji Jumanne Magembe alipotembelea mradi huo ya kukamilika
kwa mradi huo ifikapo mwishoni mwa mwezi Januari 2014 lakini bado wana wasiwasi
huenda azma hiyo isitimie kutokana na kusuasua kwa mradi huo.
Alisema kuwa CCM ndio
yenye dhamana ya wananchi na kwamba inapotokea kero kama hizo ni lazima wawe na
majibu ya uhakika ya kuwapa wananchi ili waweze kuelewa na kuendelea kukipa
dhamana chama cha Mapinduzi.
Kwa upande wake Yakoba
Madongo kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya maji wilaya ya Gairo alisema kuwa mradi
huo ulikadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.7 lakini hadi sasa
zinatarajiwa kutumika zaidi ya bilioni 7 kutokana na mahitaji mbamilmbali
yaliojitokeza ambayo awali wakati wa maandalizi ya mradi hayakuhesabiwa.
Alisema kuwa miongoni
mwa mahitaji hayo ni pamoja na tank la lita 300,000 la kuchujia maji ya
chumvi pamoja na vibanda 40 vya kuchotea maji.
Alisema kuwa hadi sasa
tayari wameshajenga matank 3, ambapo mawili ni ya uwezo wa kuchukua lita
300,000 kila moja pamoja na lenye uwezo wa kuchukua lita 1,000,000 ambalo
litatumika katika usambazaji wa maji.
Alisema kuwa mradi huo
ulikuwa ukamilike baada ya wiki 18 tangu ulipoanza, ambayo ingekuwa
Februari 2012 lakini hadi sasa bado haujakamilika kutokana na maji yaliyopatikana
kuwa ni ya chumvi na kwamba ni lazima lipatikane chujio la kuchuja maji hayo
sambamba na kuangalia ni wapi chumvi itakayopatikana baada ya maji kuchujwa itatupwa.
Alisema kuwa tatizo la
maji kuwa ni ya chumvi lingeweza kuepukwa kama wenyeji wangeshirikishwa kwani
wanajua ni eneo gani lina maji safi yasiyo na chumvi.
Katibu wa CCM mkoa wa
Morogoro Rojas Romuli aliwataka
wataalamu katika sekta mbalimbali kuwashirikisha wananchi wa eneo husika wanapotekeleza miradi ya maendeleo ili kuepuka
kutekeleza miradi isiokuwa na taija ambayo inaingizia hasara Taifa.
Hata hivyo alisema kuwa
wananchi wanatakiwa kutambua kuwa miradi hiyo ni mali yao hivyo jukumu la
ufutiliaji wa maendeleo ya miradi hiyo katika
hatua zote ni lao na siyo la serikali kama ambavyo wengi wanadhania, hali
inayosababisha miradi mingi kukwama, kuchelewa, au kutekelezwa chini ya kiwango.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni