KAMPUNI inayomiliki kitalu cha
uwindaji ya Kilombero North Safaris katika kata ya Masagati wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro
imelalamikiwa kuchoma moto nyumba sita
za wananchi, kuharibu mali zilizokuwemo ndani ya nyumba hizo sambamba
na kuwachapa viboko baadhi wamiliki wa nyumba hizo kwa madai kuwa wamevamia
eneo lao.
Wananchi hao walitoa malalamiko
hayo wakati wa ziara ya katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Rojas Romuli ya kukagua
miradi ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM pamoja na kusikiliza
kero za wananchi mkoani hapa.
Diwani wa kata hiyo Blasius Makao
alisema kuwa tukio hilo limetokea Octoba 27
ambapo zilichomwa nyumba 3, na octoba 28 zilichomwa nyumba 3.
‘’ Walifika watu wapatao 20
wakiwa na magari mawili katika kitongoji cha Igugu na Ipasile katika kijiji cha
Ipende kata ya Masagati na kufanya uharibifu huo’’ Alisema diwani huyo.
Alisema kuwa watu hao walipofika
kijijini hapo waliwachukua wajumbe wa kamati ya mazingira kwa madai ya kutaka
wakawaonyeshe mipaka ya kitalu chao cha uwindaji ambacho kipo eneo la Utengule jirani na
vitongoji hivyo.
Alisema kuwa walipofika eneo la
tukio wakawaambia wajumbe wa kamati hiyo ya mazingira kuwa eneo walikojenga
wakazi hao ni sehemu ya kitalu chao na ndipo walipoanza kufanya uharibifu huo
ambapo wenye nyumba hizo hawakuwepo, walikuwa wameenda katika shughuli zao za
maendeleo.
Diwani huyo alisema kuwa walitoa
taarifa kituo cha polisi cha tarafa ya
Milimba, polisi walifika eneo hilo na kuchukua maelezo na kwamba hakuna hatua
zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahalifu hao hadi sasa.
Pia diwani huyo alisema kuwa
walifanya jitihada za kutoa taarifa kwa mbunge wa jimbo hilo Abdul Mteketa
pamoja na mkuu wa wilaya hiyo Hassan Masala na kwamba viongozi hao hawakufika bali
kilichofanyika ni mkuu wa wilaya hiyo kumtuma afisa tarafa wa tarafa hiyo
kuangalia uharibifu huo.
Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro
Rojas Romuli aliuagiza uongozi wa CCM wilaya hiyo kuhakikisha watu hao
wanafunguliwa kesi na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
‘’ Hatuwezi kuona watu
wananyanyasika kwa stahili hii halafu tunakaa kimya, CCM ndio kimbilio la
wanyonge wanaoonewa na kunyanyaswa katika nchi hii ’’ Alisema Romuli.
Kutokana na kata hiyo ya Masagati
kutokuwa na mawasiliano ya simu wananchi hao walisema kuwa wamekuwa wakishindwa
kufikisha taarifa zao kwa wakati kwa viongozi husika ili hatua ziweze
kuchukuliwa kwa haraka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni