KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa
Wilbroad Slaa, leo, Jumatatu, Mei 13, 2013, amekaririwa na gazeti moja
akidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete na timu yake ya kampeni, “ilikuwa ikisaka kura kwenye nyumba za ibada na kumwaga sumu mbaya ya udini ambayo sasa inaitesa Serikali nataifa” kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Aidha,
katika habari hiyo iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari, “Dk. Slaa
amlipua JK” kwenye gazeti linalounga mkono CHADEMA la Tanzania
Daima,Mheshimiwa Slaa anadai kuwa migogoro ya sasa ya kidini “inajengwa
au kutengenezwa na Serikali iliyojikita kusambaza sumu ya udini katika
misikiti wakati wa kampeni za Urais mwaka 2010”.
Kwa hakika, hakuna namna nyingine ama namna bora zaidi ya kuielezea kauli hii ya Mheshimiwa Slaa isipokuwa kwamba kauli hiyo ni riwaya nyingine isiyokuwa na mshiko. Ni uongo mtupu. Yake Mheshimiwa Slaa ni maneno yasiyokuwa na ukweli wowote.
Ni uzushi na santuri ambayo
imezoeleka sasa kwa wananchi. Kauli ya Mheshimiwa Slaa ni mwendelezo wa
mtiririko usiokuwa na mwisho wa ghiriba ambazo kamwe hazitafanikiwa za
Mheshimiwa Slaa kuwahadaa wananchi ukweli wa mambo ulivyo katika nchi
yetu.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na
timu yake ya kampeni kamwe hawakufanya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010,
ama wa mwaka mwingine wowote, katika nyumba yoyote ya ibada iwe
msikitini ama kanisani ama hekaluni ama nyumba nyingine yoyote ya ibada
mahali popote katika nchi yetu.
Mheshimiwa Rais Kikwete hajawahi
hata kufikiria kuchanganya dini na siasa. Hana sababu ya kufanya hivyo.
Anaelewa fika madhara ya udini kwa mustakabali wa nchi yetu, kwa umoja
wa taifa letu na kwa mshikamno wa wananchi wake.
Yoyote
anayejaribu kumbebesha Rais Kikwete msalaba wa udini ana lake jambo na
ni vyema atuambie fika Rais alitumia Msikiti upi, ama Kanisa lipi,
mahali gani na kwa nyakati gani kufanya kampeni.
Vinginevyo,
kauli ya Mheshimiwa Slaa itabakia ni kauli tu inayostahili kupuuzwa na
wananchi, itabakia ni kauli ya mtu mzima anayetapatapa na kufanya
jitihada kubwa kujivunjia mwenye heshima kwa kutunga na kusambaza uongo.
Tunanapenda
kumshauri Mheshimiw Slaa kuwa kama hana jambo la maana lakuwaambia
wananchi ama ameishiwa na hoja ni vyema anyamaze, awaachie wananchi
waendelee na shughuli zao za maendeleo, kuliko kuendeleza riwaya zake
zisizokuwa na mshiko.Yake ni santuri iliyowachosha wananchi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Raisi Ikulu.
Dar es Salaam.
13 Mei, 2013
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni