Jumatatu, 27 Mei 2013

Pinda: Wawekezaji 45 waomba kuwekeza Mtwara


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Mtwara. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema wawekezaji 45 wameomba kuwekeza Mtwara baada ya kugundulika kwa gesi asilia mkoani humo.

Akizungumza katika sherehe za kusimikwa kwa Askofu wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kusini Mashariki, Lucas Mbedule jana Mjini Mtwara, Pinda alisema uwekezaji huo utaiwezesha Mtwara kupaa kiuchumi ndani ya miaka 10 ijayo.
“Hadi sasa kituo cha uwekezaji kina maombi takriban 45 ya wawekezaji mkoani Mtwara, ikiwamo kiwanda cha mbolea, bidhaa za plastiki… vyote hivi vitakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mtwara na Taifa kwa jumla, hususan katika ajira,” alisema Pinda.
Alisema Serikali inafahamu kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuleta maendeleo ya nchi kwa uwiano bila kubagua kwa misingi ya jinsia, rangi, kabila, dini, mikoa au ukanda… “Maendeleo ya nchi kwa uwiano ni nguzo muhimu kwa umoja na mshikamano wa wananchi wa taifa husika kama Tanzania.”

Alisema zipo nyakati ambazo baadhi ya wananchi mmojammoja au kwa makundi kama vile, jinsia, rangi, kabila, dini, mikoa na kanda wamekuwa wakiamini kuwa wanaachwa nyuma kimaendeleo na kwamba hali hiyo inasababishwa na kusubiri kwa muda mrefu na kutokupata taarifa sahihi kuhusu malengo na mipango iliyopo ya kuleta maendeleo.
“Malalamiko ya kuachwa nyuma kimaendeleo yamekuwa yakifikishwa serikalini kwa njia za barua, magazeti, majadiliano, mikutano na Bunge… lakini kwa siku za hizi karibuni ujumbe huo umekuwa ukifikishwa kwa migomo na maandamano.

Sherehe hiyo pia ilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa KKKT nchini, Dk Alex Malasusa ambaye aliwataka Watanzania kudumisha ushirikiano na kuepuka mifarakano isiyo na tija.

Askofu Mbedule alisema atahakikisha waumini wake wanakuwa kioo cha jamii katika kuhakikisha dayosisi yake inafikiwa na maendeleo ya kiroho na jamii.

Amani yaimarika

Hali ya usalama imezidi kuimarika huku Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likitumia vipaza sauti kuwataka wananchi warejee katika shughuli zao za kawaida.

Leo Waziri Mkuu anatarajia kuzuru maeneo yaliyoathiriwa na vurugu ya Magomeni, Chikongola, Reli, Nkanaledi na Mikindani kabla ya kuzindua ujenzi wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kinachojengwa eneo la Msijute.

Vurugu hizo zilizotokea Mei, 22 na 23 mwaka huu, zilichagizwa na Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuthibitisha utekelezaji wa mradi wa kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam kwa njia ya bomba watu wawili walikufa kwa kupigwa risasi na 30 kujeruhiwa.


Source: Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...