Ijumaa, 24 Mei 2013

SERIKALI YAWANYOSHEA KIDOLE WANASIASA

Serikali imesema kwamba imebaini kuwa baadhi ya wanasiasa na taasisi za kiraia wanahusika katika kuhamasisha vurugu zinazoendelea mjini Mtwara.
Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alirejea kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba Serikali itawasaka watu wote wanaohusika na vurugu hizo ndani na nje ya nchi bila kujali umaarufu na madaraka yao.
 
“Baadhi ya taasisi za kiraia na vyama vya siasa kwa masilahi yao binafsi yasiyo na upeo mpana, vinaweza kudhani kuunga mkono madai ya namna hii ni kuimarisha kukubalika kwao miongoni mwa jamii,” alisema Dk Nchimbi: “Tunawakumbusha msemo wa wahenga usemao ‘tamaa mbele, mauti nyuma’... Tunaapa kuwasaka waasisi wa vurugu ndani na nje ya Mtwara, ndani na nje ya nchi yetu.
 
Wote waliohusika kupanga, kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo hawataukwepa mkono wa sheria.”
 
Alisema Serikali inalaani vikali vurugu hizo akisema wanaozihamasisha “wataipasua nchi, watasababisha vifo vya maelfu ya watu, watajaza taifa vilema na majeruhi na hawatanufaika na matokeo haya mabaya.”
 
Dk Nchimbi alisisitiza msimamo wa Serikali kwamba maliasili hiyo ni ya Watanzania wote... “Tunalo taifa moja la Tanzania ambalo maliasili zake ni za Watanzania wote. Tabia inayoanza kujengeka ya kila eneo kutaka linufaike peke yake na mali za eneo hilo, italigawa taifa letu
vipandevipande.”
 
Alisema kiini cha vurugu hizo ni madai ya baadhi ya wananchi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam.
 
Alisema Mei 15, mwaka huu kikundi cha watu kilisambaza vipeperushi kuwataka wananchi wa huko Mei 17, saa 3:00 asubuhi kuacha shughuli na kusikiliza hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kujua mustakabali wa gesi kusafirishwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
 
Alisema juzi, makundi ya vijana yalisikiliza hotuba hiyo maeneo mbalimbali ya Mtwara kama vile sokoni, Magomeni, Mkanaredi na baadaye kupanga mawe na magogo barabarani huku wakichoma matairi.
 
“Hali hiyo iliendelea kusambaa maeneo mengine ya mji kama vile Chuno, Chikongola, Mikindani na kutoka nje ya mji hadi Mpapura, umbali wa kilomita 40 kutoka Mtwara mjini,” alisema.
 
Alisema polisi walikabiliana na vurugu hizo na hadi jana, watu 91 walikuwa wanashikiliwa.

Bajeti ya Nishati
Vurugu hizo zimemlazimu, Spika wa Bunge, Anne Makinda kuahirisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyokuwa ikijadiliwa bungeni.
Makinda aliahirisha Bunge jana asubuhi mara baada ya taarifa ya Serikali kuhusu vurugu hizo kuwasilishwa, akisema mjadala wa wabunge wakati huu unaweza kuchochea vurugu hizo.
Alisema leo Bunge litaendelea na ratiba yake kwa Bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwasilishwa.
Wanasiasa wanena
Akizungumzia vurugu hizo, Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), Samuel Sitta aliwataka Wanamtwara kutafakari faida wanazopata kwa kupinga mradi huo badala ya kukubali kutumika bila faida yoyote kwao.
“Hebu fikiria wenzetu wa Morogoro nao waseme kuanzia leo umeme wetu wa Kihansi na Kidatu hautoki nje itakuwaje? Ama sisi wa Tabora tunaolima tumbaku kwa nusu karne sasa lakini hatuna hata kilomita moja ya lami tuseme? Nchi haiwezi kuendeshwa vipandevipande.”
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini ametahadharisha hali inayoanza kujitokeza ya watu kutuhumiana kwamba fulani anahusika, akisema italigawa zaidi taifa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Diroda Babati Vijijini, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema hayo ni matokeo ya kuchezea jipu ambalo lilipaswa kutumbuliwa muda mrefu kwa kukaa, kuwasikiliza na kuwashirikisha wananchi katika masuala ya uwekezaji wa gesi.
Mbunge wa Bariadi Mashariki na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo ameitaka Serikali kuhakikisha inawasaka wahusika wa vurugu hizo kwa kuwa nchi haiwezi kuendeshwa vipande... “Ila naamini pale Mtwara tatizo siyo gesi, kuna kitu nyuma ya pazia. Kama tatizo ni gesi, wanataka nini? Gesi haimsaidii mtu yeyote mpaka iuzwe na soko lake liko Dar es Salaam ambako ndiko kwenye kampuni zinazofua umeme. Ukiizuia itakusaidiaje?
Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa aliitaka Serikali kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa huko na kusikiliza kilio chao kabla ya kuanza kulaumu. Alisema gesi ni mali ya taifa na inapaswa kutumiwa na Watanzania wote, lakini maoni ya wakazi wa huko ni muhimu pia ili kujua matakwa yao.

Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliitaka Serikali isitumie nguvu kuzima vurugu hizo la sivyo itakuwa inakoleza moto.
Alilitaka Bunge kupitia Kamati ya Uongozi, kuisimamia Serikali kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na mgogoro huo unamalizwa kwa amani.
Wahariri walaani
Jukwaa la Wahariri wa Tanzania (TEF), limelaani vikali vurugu hizo.
Aidha, TEF imesema baadhi ya vyombo vya habari viliandika au kutangaza habari za mgogoro huo katika hali iliyoashiria ushabiki na kwamba jana walikosoana na kuweka msimamo wa pamoja wa namna ya kuripoti taarifa hizo kwa masilahi ya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema wanalaani vurugu hizo kwa kuwa zinalenga kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.
“Tunalaani kwa nguvu zote kwa sababu njia wanayoitumia ya kuharibu mali na kusababisha vurugu haifai, wakiachwa waendelee nchi hii haitakalika kwa kuwa kuna makundi ya watu wengi ambao wana madai mbalimbali dhidi ya Serikali, nao wakiamua kufuata njia hiyo amani haitakuwepo kabisa,” alisema Makunga.
Alisema TEF pia imeangalia pia usalama wa waandishi wa habari wanaofanya kazi katika eneo hilo na kubaini kuwa ni hatari kwa maisha yao kwa kuwa wamekuwa wakisakwa na mwingine amechomewa moto nyumba yake, hivyo wamewasiliana na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mtwara na kushauriana nao jinsi ambavyo wanapaswa kuwakumbusha wafanye kazi zao kwa tahadhari.
Katibu Mkuu wa TEF, Neville Meena alisema wamekubaliana kuwa pia mgogoro huo ufanyiwe utafiti wa kina kwa kuwa vurugu Mtwara zimejirudia, hasa baada ya watu kujisahau na kuamini kuwa baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuzungumza na wananchi huko walimwelewa.

:::::MWANANCHI:::::

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...