Jumatano, 17 Julai 2013

SERIKALI YASAINI MKATABA KUUNDA MFUMO WA UTOAJI HUDUMA ZA KITABIBU KWA NJIA YA ELEKTRONIKI NCHINI

Jengo-la-Wodi-ya-Wazazi-Muhimbili

Na James Katubuka
Serikali kupitia Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma imesaini mkataba  kwa ajili ya kuunda mfumo wa kutoa huduma za kitabibu kwa njia ya elektroniki ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati.
Akisaini mkataba huo leo,Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. George D. Yambesi alisema mkataba huo utawezesha kuboresha huduma katika sekta ya afya nchini.
“Mfumo huu unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika huduma za kitabibu zitolewazo na Sekta ya Afya” alifafanua Bw. Yambesi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Marina Njelekela alisema, kupitia mfumo huu huduma za kitabibu zinaweza kutolewa na Daktari Bingwa aliyepo Muhimbili kwa wagonjwa walio katika hospitali zilizo katika maeneo mengine bila ya wagonjwa hao kupewa rufaa ya kuja kupata huduma hiyo Muhimbili.

“Mfumo huu utawawezesha madaktari kubadilishana ujuzi wa kitabibu kwa urahisi zaidi hivyo kuboresha huduma za afya nchini” alifafanua Dkt. Njelekela.
Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya kutoa ushauri elekezi, Meneja  Mradi  wa Swiss Tropical and Public Health Institute Bw. Reinhold Werlein aliitaka Serikali kutoa ushirikiano ili kufanikisha matumizi ya mfumo huo.
“Mshauri mwelekelezi pekee hawezi kuuwezesha mfumo huu kufanya kazi kwa ufanisi hivyo ametoa wito kwa Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha ili mfumo huu uweze kuwa na manufaa kwa watanzania” alisisitiza Bw. Werlein.
Uwepo wa mkataba huu kwa ajili ya kuunda mfumo wa kutoa huduma za kitabibu kwa njia ya electroniki ni mojawapo ya jitihada za Serikali katika kuboresha huduma katika sekta ya afya nchini.
Mkataba huu umesainiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na kampuni elekezi ya Swiss Tropical and Public Health Institute.
Mwandishi wa habari hii ni Afisa Habari Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...