Jumanne, 16 Julai 2013

SERIKALI YAWAPONGEZA WAANDISHI WA HABARI KWA KAZI NZURI

habari 1Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa akifungua mkutano kati ya Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari jijini Dar es salaam leo kushoto ni msemaji wa Wizara hiyo Bw. Godlease Malisa na kulia ni Prof. Elisante Ole Gabriel wa Wizara hiyohabari 3Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Bw. Godlease Malisa akizungumza na vyombo vya habari juu ya utekelezaji wa azma ya Serikali kusaidia Vijana, jumla ya shilingi Bilioni 6.1 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2013 kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari jijini Dar es salaam leo, kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.
……………………………………………………………………………..
Tunatambua kwamba hivi karibuni Serikali ilipitisha bajeti yake kwa ajili ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo Vijana ambayo imekuwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa ajira,hata hivyo Serikali imekuwa ikifanya jitihada za makusudi ili kuhakikisha inamkwamua kutoka katika janga la umasikini.
Katika kutekeleza azma ya kusaidia Vijana, jumla ya shilingi Bilioni 6.1 zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2013 ikiwa ni kwa ajili ya kusaidia mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambapo Vijana watapatiwa mikopo yenye unafuu katika riba na upatikanaji wake. Natoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa hii ambayo haimuhitaji mkopaji kuwa na dhamana isiyo hamishika bali kuwa na uaminifu wa kurejesha mkopo huo na kujiunga kwenye SACCOS.
Kwa kutambua umuhimu wa vijana katika maendeleo ya taifa letu, Serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana mnamo mwaka 1993/94, chini ya Sheria Na. 21 ya mwaka 1961 kifungu cha 17(1), ukiwa  na lengo la kuwasaidia Vijana kupata mikopo yenye masharti nafuu na kuwajengea uwezo kiuchumi  ili waweze kuanzisha au kuimarisha miradi yao kwa lengo la kuwawezesha kujitegemea na kukuza uchumi wa nchi.
Takwimu zinaonyesha kuwa kuna jumla ya Vijana milioni 16,195,370 ambapo takribani vijana 1,200,000 humaliza elimu ya vyuo mbalimbali kila mwaka na kati yao ni vijana 200,000 huajiriwa kwa mwaka. Ikumbukwe kuwa Vijana wanachukua asilimi 68 ya nguvu kazi ya Taifa lakini takwimu zinaonyesha kuwa upungufu wa ajira kwa Vijana ni asilimia 14.4.
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuendesha mfuko huu tayari imeshapeleke muongozo mpya wa namna bora ya vijana kunufaika na mikopo katika Halmashauri zote nchini. Hivyo Vijana mnashauriwa kujiunga katika vikundi na kufanya mawasiliano na Maafisa Vijana katika Halmashauri zenu ili kujua taratibu za kupata mikopo hiyo.
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano SerikaliniBw. Godlease Malisa ametumia fursa hii kuwapongeza waandishi wa habari kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhabarisha umma hasa katika matukio makubwa yaliyotokea hivi karibuni nchini kwetu. Mmefanya kazi kubwa sana ya kutangaza mabadiliko ya ratiba ya Bunge la Bajeti kutoka Juni – Agosti na kuwa Aprili hadi Juni kila mwaka. Kadhalika mlitangaza ziara ya Rais Obama, ziara ya Rais wa Sri Lanka, Mkutano wa Smart partnership na Maonyesho ya Sabasaba.
Serikali imepokea kwa msikitiko kifo cha mwandishi mkongwe marehemu David Majebele aliyefariki jana alfajiri na msiba upo nyumbani kwake Sinza Plot Na. 262 Block E, Mtaa wa Lion Hotel, ambapo mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Alhamisi katika makaburi ya Kinondoni. Wizara inatoa pole na salam za rambirambi kwa ndugu, jamaa na familia ya Marehemu, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi AMINA.
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilianzishwa mwaka 2006. Wizara hii inaundwa na Idara nne za kisekta ambazo ni Idara ya Habari, Idara ya Maendeleo ya Vijana, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni na Idara ya Maendeleo ya Michezo.
Imetolewa na
Bw. Godlease Malisa
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...