CHAMA cha Mapinduzi CCM Mkoa wa
Morogoro Kimeitaka serikali kuwachukulia hatua watendaji wa idara ya kilimo wilayani Kilombero waliohusika kufanya
ubadhilifu kwa kujenga mradi wa skimu ya umwagiliaji eneo ambalo halikustahili
na hivyo kuitia hasara ya shilingi milioni 700.
Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro
Rojas Romuli alisema hayo jana wakati alipotembelea katika mradi huo uliopo
katika kijiji cha Signali kata ya
Kiberege wilayani Kilombero, akiwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Romuli alisema kuwa kwa mradi
mkubwa kama huo ni lazima ungefanyika utafiti wa kina ili kubaini kama eneo hilo
linafaa kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, kwa kuzingatia upatikanaji wa maji ya
uhakika.
Kwa upande wake diwani wa kata ya
Kiberege ulipojengwa mradi huo, Ramadhani Makung’uto alisema kuwa mradi huo ulipowasilishwa katika
baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo waliukataa kutokana na kwamba
walijua hautakuwa na tija kwa sababu eneo hilo halina maji kwa muda wote kama
ambavyo inastahili kwa mradi wa aina hii.
‘’ Mradi huu madiwani walikukataa,
kilichotokea ni kwamba wataalamu wa kilimo wa kanda ndio waliolazimisha mradi
ukajengwa katika eneo hilo na sasa hauna tija. Kwa mradi huu fedha za wananchi
zimepotea bure’’ Alisema.
Wataalamu hao wametajwa kuwa ni
Injinia Joshi Chum na mwingine aliyetambulika kwa jina moja la Injinia Mlelwa
kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Mwenyekiti CCM wilaya ya
Kilombero Abdalla Kambangwa alisema kuwa
aliyekuwa Afisa maendeleo ya kilimo
na mifugo Mary Kitua ambaye kwa sasa amehamishiwa wilaya ya Ngorongoro
ndiye aliyehusika na usimamizi wa mradi huu na amekwamisha miradi mingine mingi
mingi katika wilaya hiyo ikiwemo ya
umwagiliaji , majosho, maghala ya kuhifadhia mazao pamoja na masoko.
‘’ Katika miradi mingi ambayo
tumeitembelea tumebaini imekwama, na kila mwaka katika bajeti zinaonyesha kuna
fedha zimetengwa kwaajili ya miradi kama hiyo ambayo haikamiliki’’.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa
ukaguzi wa fedha za miradi hiyo ulishafanyika na kwamba hadi sasa bado ripoti
haijatolewa jambo ambalo wananchi wanalilalamikia.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Morogoro
Rojas Romuli ametaka hatua zichukuliwe dhidi ya Afisa aliyefanya ubadhilifu wa
mamilioni ya fedha za miradi ya kilimo na mifugo katika wilaya hiyo ambaye kwa
sasa amehamishwa katika wilaya nyingine jambo ambalo sio sahihi, na kwamba
inafaa awajibishwe.
Pia ametaka hatua zichukuliwe
dhidi ya wataalamu waliolazimisha mradi huo kujengwa katika eneo ambalo
halistahili na kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma.
Mwisho
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni