Jumapili, 24 Novemba 2013

WALIMU WAGEUZWA KUWA WATENDAJI WA VIJIJI KILOMBERO

WAZAZI wilayani  Kilombero mkoani Morogoro wameitaka serikali kuacha kuwatumia walimu wakuu kukaimu nafasi za utendaji wa kijiji  hali inayosababisha walimu hao kushindwa kufanya majukumu yao ya elimu.

Wazazi hao walisema hayo jana wakati wa ziara ya katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Rojas Romuli alipotembelea wilayani kilombero katika ziara yake ya kikazi.

Mmoja wa wazazi hao  Agatuni Malilima mkazi wa kata ya Kisawasa akizungumza kwa niaba ya wenzake  alisema kuwa ni lazima serikali ichukue hatua za haraka kuajiri watendaji wa vijiji ili kuepuka adha hiyo ambayo inapelekea kushuka kwa elimu wilayani humo.

‘’ Tatizo hili ni sugu katika maeneo mbalimbali Huku Kilombero, unakuta mtendaji wa kijiji yupo mmoja tu katika vijijiji 6 ambapo wengiene wote wanaokaimu ni walimu’’ Alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero David Ligazio alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba linatokana na ajira zote za watumishi wa serikali zinatoka tume ya utumishi wa umma.

‘’ Ni kweli upo upungufu mkubwa wa watumishi hao, tulishapeleka kero hii lakini bado haijashughulikiwa’’ alisema mwenyekiti huyo.

Aidha alisema kuwa waliomba waziri wa wizara husika kusaini kanuni ambazo zitawapa fulsa ya kuajiri watumishi wa  nafasi za ngazi za chini ili kupunguza kero hiyo.

Alisema kuwa kero hiyo sio kwa watendaji tu bali hata katika sekta ya afya na kwamba wauguzi waliopo hawakidhi mahitaji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...