Ijumaa, 8 Novemba 2013

RAIS KIKWETE ALIHUTUBIA BUNGE DODOMA

Na  Magreth Kinabo
 
Rais Jakaya Kikwete amesema kwamba Tanzania  haina mpango wa kujitoa  katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na  itaendelea kuwepo kwa kuzingatia matakwa ya mkataba wa EAC na Itifaki zake,licha ya kutoshirikishwa kwa baadhi ya mambo.
 
Aidha   Rais   Kikwete  amesisitiza   kuwa  Tanzania ni kati ya zile  nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja na kuongeza kuwa huo sio msimamo wake au Serikali pekee   bali ndio Watanzania walio wengi.
 
Kauli hiyo ilitolewa leo Bungeni  mjini Dodoma wakati Rais Kikwete alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu msimamo wa Tanzania juu ya EAC.
 
“Napenda kuwahakikishia  waheshimiwa  wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa).  Tupo na tutaendelea kuwepo!,” Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za EAC na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki .
 
“Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa jumuiya haidhoofiki wala kufa.  Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake.  Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa EAC  inaendelea kustawi,” alisema Rais Kikwete.
 
Alisema kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake,   ilieleza kuwa asilimia 74.4  ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake.
 
Rais  Kikwete alisema  ni lazima ni kutambua ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa EAC.
 
Alisema  Tanzania itaendelea kukumbusha umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa, kama vile kuheshimu matakwa na masharti ya mkataba ulioanzisha EAC, Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za jumuiya  hiyo .
 
“Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake,” alisisitiza.
Rais Kikwete.
 
Alisema    msimamo  na mtazamo  wa nchi , kuundwa  kwa Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho.
 
Akizungumzia kuhusu  kumekuwepo  na madai  Tanzania inachelewesha  maendeleo ya jumuiya   hiyo   alisema  hayana ukweli wo wote.
 
Huku akiongeza  Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini inapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla hazijakamilika.   Hivyo  alizitaka nchi uanachama  kuwa makini  katika kila hatua tunayochukua.
 
 Alisema   kwa msimamo na mtazamo  wa nchi ,  suala  la Shirikisho  liwe  ndiyo hatua ya mwisho.
 
 Hata hivyo Rais Kikwete alisema  pengine msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji,ndiyo yanayotuletea vikwazo.
 
 Hivi karibu  viongozi wa nchi tatu wanachama wa EAC  yaani Uganda, Rwanda na Kenya walikutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi.  Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani Juni  24-25 , 2013 mjini Entebbe, Uganda; Agosti  28, 2013 mjini Mombasa, Kenya na Oktoba 28 , 2013 mjini Kigali, Rwanda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...