Jumanne, 19 Novemba 2013

WATU 500 WAUGUA UGONJWA WA MATUMBO NA KUHARA KWA KUKOSA MAJI





WATU 500 wameugua ugonjwa wa matumbo na kuharisha katika kata ya Lupilo wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro kutokana na tatizo la maji.
 

Mganga mfawidhi katika kituo cha afya cha Lupilo Beltod Malongo amesema hayo Novemba 19 mwaka huu wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa chama cha mapinduzi CCM waliotembelea  katika kituoni hapo kujionea huduma za afya.

Aidha Dk huyo alisema kuwa watu hao wameugua magonjwa hayo katika kipindi cha mfululizo wa miezi 3 kuanzia Septemba hadi sasa ambapo amesema kuwa magonjwa hayo husababishwa na ukosefu wa maji safi na salama.

Dk huyo amesema kuwa tatizo hilo pia limekuwa likiathiri utendaji kazi katika kituo hicho  kutokana na kwamba mtoa huduma anatakiwa kutumia maji safi kabla na baada ya kuwahudumia wagonjwa jambo ambalo katika kituo hicho  ni kikwazo.

Kwa upande wa wakazi wa kata hiyo wamesema kuwa tatizo hilo ni kubwa na kwamba kama serikali haikuchukua hatua za makusudi wananchi hao wataendela kutaabika na kupata magonjwa ya milipuko mara kwa mara.

Mmoja wa wakazi wa kata hiyo Said Liepa amesema kuwa kwa sasa dumu la lita 20 ya maji wananunua kwa shilingi 500  kiasi ambacho wananchi wa kipato kidogo wanashindwa kumudu na hivyo kutumia maji ya madimbi ambayo si salama.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ulanga  Furaha Lilongeli amesema kuwa tayari serikali imeshaanza kutekeleza mradi wa maji katika kata hiyo ambao ni ahadi ya rais Kikwete wakati  alipotembelea katika kata hiyo na kuambiwa kero hiyo na kuahidi kuitatua.

Amesema kuwa mradi huo  unagharimu kiasi cha shilingi milioni 396.8 na kwamba kwa sasa upo katika hatua za mwisho na ujenzi wa matank ya maji.



Katibu wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro Rojas Romuli ameutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ulanga kuhakikisha inatatua tatizo la maji kwa kukamilisham radi mkubwa wa maji unaojengwa katika kata hiyo haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha ya watu hao,
Mwisho

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...