Alhamisi, 5 Desemba 2013

TAARIFA KUTOKA IKULU KUHUSU RAIS JAKAYA KIKWETE



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wiki hii atahudhuria mikutano miwili mikubwa ya kimataifa ukiwamo wa kujadili amani na usalama Barani Afrika kwa mwaliko wa Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Rais Kikwete ambaye aliondoka nchini usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Desemba 4, 2013, atakuwa mmoja waviongozi wa Afrika ambao watahudhuria Mkutano Kati ya Marais wa Afrika na Ufaransa, ambao utafanyika kwa siku mbili katika Kasri ya Elysee mjini Paris kuanzia keshokutwa Ijumaa, Desemba 6, 2013.
Mkutano huo uliopewa jina la Elysee Summit utakuwa ni mkutano wa 26 wa Mikutano ya Wakuu wa Nchi za Afrika na Ufaransa ambao walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 1973 kwa madhumuni ya kuzikutanisha Ufaransa na makoloni yake ya zamani katika Afrika.
Kwa mikutano miwili ya kwanza, washiriki walikuwa ni marais wa nchi za Afrika zilizokuwa makoloni ya Ufaransa lakini mwaka 1976 zilialikwa nchi zinazozungumza lugha ya Kireno katika Afrika kama watazamaji tu.
Mwaka 1981 jina na madhumuni ya mkutano huo yalibadilika na ukaanza kuitwa The Conference of Heads of States and Government of Africa and France na mwaka 1996 mkutano huo ulifunguliwa kwa nchi zote za Afrika bila kujali zinazungumza lugha gani. Awali mkutano huo ulikuwa unafanyika kila baada ya miaka miwili, sasa ni kila baada ya miaka mitatu.
Kama ilivyokuwa mkutano uliopita uliofanyika mwaka 2010 mjini Nice, Ufaransa, mada kuu ya Mkutano huo ni kujadili amani na usalama katika Bara la Afrika vikiwemo vita ndani ya nchi mbalimbali, uharamia kwenye bahari, biashara ya dawa za kulevya, ugaidi na ujambazi wa vikundi na jinsi mambo hayo yanavyoathiri Afrika na Ufaransa.
Aidha, Mkutano huo utajadili mada nyingine mbili ambazo ni Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Rais Kikwete na mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Hollande watakuwa Wenyeviti-Wenza wa kikao kitakachojadili madhara ya Mabadiliko ya Tabia Nchi. Rais Kikwete atakuwa Mwenyekiti-Mwenza wa kikao hicho katika nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU)Juu ya Mabadiliko ya Tabia Nchi (CAHOSCC).
Rais Kikwete anatarajiwa kuwaeleza viongozi wenzake matokeo ya Mkutano wa COP19/CMP9 uliofanyika karibuni mjini Warsaw, Poland kujadili suala zima la Madhara ya Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Mkutano mwingine mkubwa ambao Rais Kikwete atahudhuria ni ule wa marais wa Afrika utakaojadili jinsi ya Jumuiya ya Kimataifa inavyoweza kushirikiana kukomesha ujangili na biashara haramu ya pembe za tembo na faru.
Katika Mkutano huo utakaofanyika Hoteli ya de la Marine, Rais Kikwete aanatarajiwa kuwaeleza viongozi wenzake kuhusu hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali yake kukabiliana na ujangili nchini chini ya Operesheni Tokomeza.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

4 Desemba, 2013

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...