Jumatatu, 4 Agosti 2014

MAPOROMOKO YA SANJE YAUA MWANAFUNZI WA SEKONDARI



 
MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Mwandege mkoani Pwani Samuel Aliko (18), amefariki dunia baada ya maji aliyokuwa akiogelea katika maporomoko ya Sanje wilayani Kilombero mkoani Morogoro kumshinda nguvu.
 
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani hapa Leonard Paulo tukio hilo lilitokea Agosti 2 mwaka huu, saa 7 mchana katika eneo la Sanje tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero.
 
Kamanda Paulo alisema kuwa kwa mujibu wa mwalimu wa shule hiyo Shauri Abel (33) mkazi wa Pwani alidai kuwa akiwa kwenye mafunzo na wanafunzi wake wakiogelea kwenye maporomoko hayo ya Sanje ndipo mwanafunzi huyo alifariki dunia baada ya maji kuzidi nguvu.
 
Kamanda huyo alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ya maji ni maji kumshinda nguvu na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea.
 
Wakati huo huo mlinzi mmoja Pius Mbuya (45) mkazi wa mlali wilayani Mvomero amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akivuka barabara.
 
Kamanda Paulo alisema ajali hiyo iliyokea agosti 3 mwaka huu, saa 1:45 usiku katika eneo la njia panda ya kichangani barabara ya zamani ya Dar es salaam.
 
Alisema, gari lenye namba za usajili T 444 CKK iliyokuwa ikiendeshwa na Selestina Nkelehe (43) mkazi wa DSM ikitokea Bigwa kwenda mjini kati ilimgonga mlinzi huyo ambaye alikuwa amepanda baiskeli na kusababisha kifo chake papo hapo.
 
Alisema kuwa mtuhumiwa amekamatwa na chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa gari hiyo.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...