Jumanne, 4 Juni 2013

RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, DKT. SHEIN AREJEA ZANZIBAR KUTOKA CHINA

IMG_2453
NA RAMADHANI ALI /HABARI MAELEZO ZANZIBAR                          
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Muhammed Shein amesema ziara yake ya wiki moja nchini China itaisaida sana Zanzibar katika  kuimarisha uhusiano kati ya nchi hiyo na Zanzibar  na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Dk. Shein amesema katika ziara hiyo amefanya  mazungumza na viongozi wa juu wa China akiwemo Rais, Makamu  wake na Waziri Mkuu wa  nchi hiyo  ambayo yalilenga  kuimarisha uchumi wa Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo.
Amezitaja sekta hizo kuwa ni pamoja na Afya, Kilimo, Huduma za Elimu na Biashara pia waliangalia uhusiano katika maeneo mengine mapya ya uvuvi wa bahari kuu na uwekezaji vitega uchumi.
Dk. Shein amesema China na Zanzibar wamekubaliana  kuimarisha sekta ya Biashara ambapo Naibu Waziri wa Biashara wa China ameitaka Zanzibar kuandaa rasimu ya mapendekezo ya miradi ambayo itashughulikiwa  na nchi yake.
Akizungumzia  Kilimo Rais  Shein amesema wamekubaliana na China kuja  kufanya utafiti wa uvuvi wa  bahari kuu, kusaidia utaalamu na  kuwekeza miradi mikubwa katika sekta hiyo.
“ Uvuvi unanafasi kubwa katika maendeleo ya Zanzibar lakini tunahitaji uvuvi wa kisasa wenye tija, na kuanzisha miradi ya ufugaji samaki na yote haya wenzetu wamekubali, ” amesema Dk.Shein.
Amesema  Zanzibar imepeleka wavuvi wadogo wadogo 59  wa vijiji vya  Unguja na Pemba kujifunza nchini China na waliporudi wamewaelimisha  wavuvi wenzao  na tayari mafanikio yameanza kuonekana.
Ameongeza kuwa katika mazungumzo yake na viongozi wan chi hiyo amewataka kuimarisha sekta ya Utalii kwa kuitangaza Zanzibar na kuwashajiisha wananchi wa nchi hiyo kufanya ziara za kitalii nchini.
Rais wa Zanzibar amesema katika kufanikisha ziara  hiyo Ujumbe mkubwa kutoka China utawasili Zanzibar muda mfupi ujao kuangalia maeneo ya uwekezaji na ametaka wahusika kujiandaa.
“Lazima tubadilike na tujiandae wenzetu hawako katika mchezo katika uwajibikaji na ndio maana nchi yao inapiga hatua kubwa ya maendeleo, ” amesema Rais wa Zanzibar.
Akizungumzia ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Zanzibar uliokuwa ukifanywa na Kampuni ya Ujenzi kutoka China na ambao umekwama, Dk. Shein amesema yapo mategemeo makubwa ya kuanza tena muda mfupi ujao baada ya mshauri muelekezi alieletwa na Zanzibar kutoka Ufaransa kukamilisha kazi yake.
Dk. Shein na ujumbe wake waliondoka Zanzibar tarehe 27 mwezi uliopita na katika ziara hiyo aliungana na viongozi wengine kutoka  Sirilanka, Papua New Guinea, Singapore na Malaysia  katika mkutano mkubwa wa Kimataifa wa Biashara uliofanyika nchini humo.                                 
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...