Jaji
Warioba – Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph
Warioba akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo
(Jumatatu, Aprili 29, 2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid.
(Picha na Tume ya Katiba).
Na Mwandishi Wetu
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kuandaa rasimu ya katiba
itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na
kutoa maoni yao katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi
Juni mwaka huu (2013).
Mwenyekiti
wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema leo (Jumatatu, Aprili 29,
2013) jijini Dar es Salaam kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake
haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.
“Tume
haitengenezi katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa katiba ya nchi,”
amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa habari katika
ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja
zilizotolewa na wananchi na sio idadi ya watu waliotoa maoni.
Jaji
Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi,
taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya
katiba ya wilaya.
Walemavu
– Mwenyekiti wa kamati ya uwasilishaji wa mapendekezo ya muundo wa
mabaraza ya Katiba kwa jamii ya watu wenye ulemavu, Bw. David Nyendo
(kushoto) akiwasilisha maoni yake ya kamati hiyo kwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba katika mkutano baina yao uliofanyika ofisi za Tume Jijini Dar
es Salaam tarehe 13 Feb mwaka huu (2013). Kulia ni Mjumbe wa Tume, Dkt.
Salim Ahmed Salim. (Picha na Tume ya Katiba).
Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu
Akizungumza
kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba
amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye
ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa
maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.
Hatua hii
inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania
(SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA)
waliloliwasilisha kwa Tume.
Jaji
Warioba amesema Baraza moja litaundwa Tanzania Bara na jingine Zanzibar
na kwamba yatashirikisha wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi
Taifa.
“Tunaelewa
kuwa watu wenye ulemavu ni karibu asilimia 10 ya watanzania wote na
mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi yoyote,” amesema Jaji
Warioba na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake inazo zinaonyesha
baadhi ya watu wenye ulemavu wamependekezwa na mitaa, vijiji, vitongoji
na shehia kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Chaguzi za Wajumbe Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Aidha, Jaji
Warioba amezungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika
chaguzi zilizofanyika nchini kote hivi karibuni za kuchagua Wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia.
Kwa mujibu
wa Jaji Warioba, tathmini ya Tume inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa
viongozi na watendaji katika ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata
walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi
walichaguana kwa amani na utulivu.
“Kwa mfano
jumla ya shehia 323 sawa na asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa upande
wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato huu, hali kadhalika jumla ya
Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya Kata 3,339 kwa Tanzania Bara
nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa Mwongozo,”
amesema Jaji Warioba.
Kuhusu
hatua inayofuata baada ya chaguzi hizo, Jaji Warioba alisema Tume
inaendela kupokea majina kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na ya
wananchi wote waliopendekezwa kutoka katika Kata na Shehia na kazi hiyo
inatarajia kukamilika ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu (2013).
Changamoto
Akizungumzia
kuhusu changamoto zilizojitokeza katika chaguzi hizo, Jaji Warioba
amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana pia kulijitokeza
changamoto kadhaa ambazo zilisabishwa na misimamo ya kisiasa na kidini
“Katika
baadhi ya maeneo mikutano ya uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia
ilishindwa kufanyika kutokana na mivutano ya kisiasa na kidini
zilizosababishwa na baadhi ya wananchi kufangamanisha chaguzi za Wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na masuala ya kisiasa na kidini,”
amesema Jaji Warioba.
Jaji
Warioba ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi
kujiingiza katika vitendo vya rushwa katika chaguzi hizo ili
wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo ya katiba.
“Tumepokea
pia malalamiko ya vitendo vya rushwa,” alisema Mwenyekiti huyo na kusema
vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kuongeza kuwa taasisi zenye
mamlaka ya kupambana na vitendo hivyo zinapaswa kushughulikia malalamiko
hayo.
Aina na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba
Katika
mkutano huo uliofanyika katika katika Ofisi za Tume zilizopo mtaa wa
Ohio jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti huyo pia alizungumza kuhusu aina
na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.
Kwa mujibu
wa Jaji Warioba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa
ya kuundwa kwa mabaraza ya aina mbili ambayo ni Mabaraza yatakayoundwa,
kusimamiwa na kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe itakayopangwa na
Tume.
Aina ya
pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni Mabaraza ya Katiba ya Asasi,
Taasisi na Makundi mbalimbali yenye malengo yanayofanana. Mabaraza haya
yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha yenyewe na kisha kuwasilisha
maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.
“Kazi kubwa
ya Mabaraza ya Katiba ya aina zote mbili ni kuipitia, kuijadili na
kuitolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume kutokana
na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,” alisema Jaji Warioba na
kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama mbalimbali kutumia fursa hiyo
ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba
itakayotolewa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni