NAIBU Waziri wa Kilimo, Adam Kighoma Malima atakuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Wasanii Mastaa litakalofanyika Juni 29, mwaka huu kwenye kijiji cha Mwanzega, Mkuranga mkoa wa Pwani.
Akizungumza na viongozi wa Mtandao wa Wasanii (SHIWATA) mjini Dodoma katika vikao vya Bunge vinavyoendelea, Malima alisema amekubali kuwa mgeni rasmi vile vile tukio hilo linafanyika katika jimbo lake la uchaguzi la Mkuranga.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Caasim Taalib alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na kuongeza kuwa kutakuwa na matukio ya wanachama kukabidhiwa nyumba zao kwa wale waliomaliza michango yao akiwemo mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,Jellah Mtagwa atakabidhiwa nyumba yake.
Alisema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida ambaye alikuwa mgeni rasmi tamasha lililopita Mei mwaka huu Dar es Salaam na kuahidi kukarabati barabara za kuingia kijiji cha wasanii Mkuranga atakabidhiwaq kadi pia taasisi yake ya ujasiriliamali ambayo itawakopesha wasanii wa SHIWATA sh. Bil. 7 kwa ajili ya kuendeleza wasanii, itaanza kutekeleza mpango huo wa Awamu ya Kwanza siku hiyo.
Alisema mbunge wa Kinondoni Bw. Idd Azzan naye atakabidhiwa kadi ya kujiunga na SHIWATA ambako pia wabunge mbalimbali wamealikwa kuhudhuria tamasha hilo akiwemo mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu.
Wabunge wengine wa mkoa wa Dar es Salaam walioalikwa katika tamasha hilo ni John Mnyika wa Ubungo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR- Mageuzi , James Mbatia.
Alisema mtandao wa SHIWATA ambao umekuwa ukiandaa matamasha ya wasanii kila mwezi limepeleka tamasha la Juni kwenda wilaya ya Mkuranga ambako ndiko zinakojengwa nyumba zao katika kijiji cha Mwanzega-Kimbili ambako mpaka sasa watu nane watakabidhiwa nyumba zao.
Wasanii 400 kutoka vikundi mbalimbali vikiwemo vya mkoa wa Pwani wanatarajiwa kushiriki katika tamasha hilo.
Wanachama wa SHIWATA nao wanakaribishwa kuhudhuria tamasha hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni